SITOKUSAHAU.
SEHEMU YA-01.
Nguvu ya mapenzi inaweza kukufanya uyapuuzie maneno ya watu waliokuzidi umri sana sana wazazi wako ama marafiki zako.Mzazi anaweza kukwambia achana na huyu hakufai lakini wewe ukapinga na yote hii ni kwasababu umependa kupita kawaida.Cha ajabu yule uliye mpenda iwapo akikutenda Basi hapo hapo unaanza kuyakumbuka maneno ya wazazi wako au ndugu wengine waliokushauri hapo awali."Ningejua" Ni neno pekee ambalo linaweza kubaki kichwani mwako iwapo ukitendwa..
ANZA NAYO👇
“Karibu sana mwanangu,pole sana na masomo pia na changamoto zingine.Jisikie upo huru mwangu lakini yakupasa kuwa makini sana mwanangu.Dunia ya sasa hivi imeharibika sana sio kama zamani,kila kitu kiko ovyo ovyo kabisa,vitu vingi vimebadilika pamoja na magojwa yasababishwayo na zinaa yanazidi kuongezeka.Hivyo mwanangu Tony jichunge sana hasa kwa mtu kama wewe uliyetoka mjini”Ilikuwa ni sauti ya mama mmoja aitwaye Pudensia akimwambia mwanaye aliyekuwa ametoka masomoni katika chuo cha Mandaka kilichoko Moshi.Ni takribani miaka sita imepita tangu atoke kijijini kwao Mngeta,Kijiji ambacho kiko Morogoro.Tony baada ya kumaliza darasa la saba alienda Moshi kwa mjomba wake hivyo hata shule ya sekondari alisomea huko huk.Shule ya St.James ndo shule aliyosoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.Bahati mbaya kwake hakuchaguliwa kuendelea juu japokuwa yeye alikuwa na uhakika kuwa alifaulu mtihani na alikuwa na vigezo vyote vya kuendelea na kidato cha sita,
“Ati nini?nimefeli?hapana haiwezekani,tangu kidato cha kwanza nashika namba moja na isitoshe huu mtihani haukuwa mgumu kwangu na nilitegemea nitapata hata grade A.Ila naimani kuna kitu kimefanyika hapa.Nasema tena hata kama mtihani wanaurudisha naufanya vizuri hata kama natoka usingizini” Yalikuwa ni maneno ya Tony akiyaongea kwa jaziba pale alipoyaona matokeo kuwa kashinda kwa kiwango cha kuanza kutafuta chuo na sio kuendelea na kidato cha sita.Moyoni alijawa na hasira kupita kiasi akiamini kuna mchezo umefanyika na aliapa kuwa atalifanyia uchunguzi aweze kulifahamu kwa undani zaidi.
*
Kitendo cha kufeli kikamfanya mjomba wake aitwaye Feriginand kumtafutia chuo ambacho kilikuwa karibu na walipokuwa wamaishi.Baada ya kuingia chuoni hapo alisoma kwa bidii kubwa sana jambo lililomfanya ajitenge mda mwingi akiwa peke yake anajisomea pia alipenda kujifunza mambo mengi sana.Alisoma kwa hasira sana kwani malengo ilikuwa ni kuendelea na kidato cha sita lakini matokeo yalikuja tofauti na alivyotegemea.Moyoni aliumia sana lakini alishukuru Mungu pale alipopata nafasi chuoni hapo hivyo akauanza mwaka wa kwanza kwa juhudi ya hali ya juu sana.Kama ilivyo kawaida wanachuo kuanzisha mahusiano lakini jambo lile kwake lilikuwa ni tofauti sana.Kila mara maneno ya mjomba wake yalikuwa yakijirudia kichwani kuwa soma kwa bidii,
“Hatua ya kwanza umefeli hivyo kuwa makini sana hatua ya pili usifeli.Soma kwa bidii sana kumbuka maisha ya mama yako huko kijijini”Mjomba wake yale maneno aliyaongea kwa hisia kali pindi alipopata matokea ya Tony kutochaguliwa kuendelea.Maisha yalikuwa magumu sana kijijini kwao Mngeta,alipomaliza darasa la saba alichukuliwa na mjomba wake kwani mama yake alikuwa anahangaika na wadogo zake wawili ambao mmoja alikuwa darasa la tano huku mwingine akiwa la kwanza.Hali ilikuwa mbaya kwani hata mjomba wake Tony hakuwa na uwezo mkubwa hivyo mama yake Tony alilazimika kuuza shamba kubwa kwa ajili ya Tony ili aweze kusoma,
“Tazama mwanangu nimeuza shamba lile kubwa kwa ajili yako,jitahidi usiniangushe soma kwa juhudi kumbuka kilichokupeleka shuleni”Yalikuwa ni maneno ya mama yake kwa njia ya simu pale alipotuma hela kutoka kijijini kwenda Moshi kwa mjomba wake Tony.Kitu kinachoweza kufanya maisha yako yaendelee ama yarudi nyuma ni mapenzi.Ukisha jiingiza kwenye suala hilo unaweza kusababisha hata kile unachokifanya kiyumbe.Hivyo Tony alikuwa makini sana na suala hilo.Hadi anamaliza kidato cha nne hakuwa amejiiingiza kwenye mahusiano.Licha ya kufeli hakuwa na chochote kilichokuwa kinamsibu.Kitendo cha kuingia chuoni kilimfanya asome kwa juhudi sana kwani nafasi ya kwanza hakuwa nayo.Wadada wengi chuoni hapo walianza kujileta kwa Tony kama ilivyo kawaida yao lakini Tony aliwakwepa.Hakuwa na mazoea ya kutembea sehemu yeyote zaidi alibaki ndani ya chuo,
“Kosa la kwanza sio kosa,kurudia kosa ndo kosa.Naimani sitomwangusha tena mama yangu anaweza kufa kwa sababu ya msongo wa mawazo”Alijisemea Tony huku akijaribu kuvuta picha ya maisha ya nyumbani kwao.Alilikumbuka lile shamba kubwa lililouzwa kwa ajili yake hapo ndipo alipozidisha juhudi.Alikuwa na nidhamu ya hali ya juu sana na hii ilitokana na kutojihusisha na makundi yeyote.Miezi sita ya kwanza ikaisha akiwa bado na kasi ya kusoma ile ile.Ikaingia miezi sita mingine mambo yakawa yale yale.Juhudi yake ilizidi kuongezeka.Hakufikiria kuwa atafeli tena.Nia yake iliku wa ni kuja kuwa mwalimu wa sekondari japo alitambua vyema kuwa mshahara wake ni mdogo lakini alijisemea kuwa ile inaweza kuwa ni msingi wa kumfanya yeye apande juu.Lengo lake lile aliamini kuwa litatimia,
“Elimu haina mwisho” Alijisemea huku akiamini kuwa akishakuwa mwalimu basi ataendelea kusoma zaidi.Alizidisha nidhamu alikuwa na uwezo wa kukaa kimya masaa hata sita akiwa hajaongea neno lolote,kiufupi hakupenda sana kuongea ongea ili kuepusha mazoea na wasichana ilikuwa lazima kwake mda wote kukunja uso.Kukaa kwake kimya kulikuwa na jambo zito kichwani,kila mara alilifikiria hilo na ndo lilimzidishia kasi ya kusoma kwa bidii zote.Baba yake alifariki dunia miaka saba iliyopita.Kwa wakati huo yeye alikuwa darasa la sita akiwa na umri wa miaka kumi na mbili.Alikumbuka wakati wako porini yeye na baba yake wakikata mkaa,ndipo baba yake alipopanda juu ya mti kwa ajili ya kukata matawi.Lakini bahati mbaya kwake aliteleza na kudondoka chini kutokana na urefu wa mti aliokuwa ameupanda alipoteza maisha hapo hapo.Jambo lile lilipelekea upweke kwenye familia ile na majukumu yote yakabaki kama Pudensia ambaye ni mama yake Tony.Yote aliyakumbuka akiwa mwaka wa pili na hapo ndipo alizidisha juhudi ya kujifunza vingi lengo wakati wa kuhitimu chuo awe na vigezo vitakavyomfanya awe mwalimu wa sekondari.
*
“Asante sana mama nimekaribia,niko makini wala hata usijali kuhusu mimi.Nimeondoka hapa nikiwa na umri wa miaka kumi na tatu lakini narudi nikiwa na miaka kumi na tisa.Ndani ya miaka hiyo yote sijafanya maovu yeyote mama hivyo ondoa shaka” Tony alimjibu mama yake kisha wakaendelea kuzunguka zunguka sehemu tofauti kama kumuonyesha mazingira jinsi yalivyobadilika kwa kiasi kikubwa.Waliongea mengi siku ile,
“Mama mwembe wangu ulivyokuwa mtamu mliukata?”Aliuliza Tony ikiwa ni kama utani kwa mama yake
”ndio ushachomwa mkaa mda mrefu sana”Mama yake alimjibu kisha wakaendelea na maongezi ya hapa na pale na kwa wakati huo Tony alikuwa likizo hivyo alitakiwa kukaa pale kijini kwa mwezi mmoja kisha asafiri kurudi Moshi uendelea na masomo yake.Mama yake hakuacha kumsihi mwanaye asijiingize kwenye vitendo vitakavyomfanya aporomoke kimaadili,
“Ondoa wasiwasi mama niko makini”Alimjibu Tony lakini moyoni alikuwa na kitu kilichomsumbua sana.Mara nyingi alitamani kukisema kwa mama yake lakini alisita na kubaki nacho moyoni.Siku zilikatika na hatimaye ikabaki wiki moja ili Tony asafiri tena kurudi chuoni kuendelea na masomo yake.Aliwaaga baadhi ya ndugu na kuwahidi kuwa atarudi akisha maliza masomo yake ambayo yalikuwa yamebakiza mwaka mmoja na nusu,
“Mama..”Aliita Tony na kumfanya mama yake aliyekuwa anachambua njegere kusitisha zoezi lile na kumtazama mwanaye aliyeonekana kuwa na jambo mhimu la kuongea,
“Eeeh unasemaje?’ Mama yake alimuuliza,
“Nauchukia umasikini kupita kiasi”Aliongea Tony maneno yaliyomfanya mama amuangalie tena na kumuuliza sababu ya kuuchukia umasikini ilhali ndo maisha wanayo ishi,
“Ni jambo zito kichwani mama”Aliongea Tony,
“Jambo gani hilo?”Aliuliza mama yake….
Tony ana nini?kwanini auchukie umasikini?hiki ni kigongo kipya ndo tunakianza kwa namna hiyo nakusihi baki nami mwanzo hadi mwisho kuna mengi ya kujifunza..